Taarifa ya Mshiriki

Unaombwa kushiriki katika utafiti! Kabla ya kuamua kama ungependa kushiriki katika utafiti huu au la, ni muhimu kwako kuelewa ni kwa nini utafiti unafanywa na utahusisha nini.

Utafiti huu unahusu nini? 

Umealikwa kushiriki katika utafiti unaochunguza afya na ustawi wa Vijana mjini Mombasa. Tunahitaji maelezo kuhusu afya na ustawi wako ili kuelewa vyema jinsi ya kutoa programu za afya na kutathmini kama programu za sasa zinafanya kazi. 

Kwa kushiriki katika utafiti huu, utatoa taarifa mpya muhimu ili kusaidia afya ya Vijana hapa Mombasa.

Nani amealikwa kushiriki? 

Utafiti huu ni wa vijana wenye umri wa miaka 10-24 ambao wako Mombasa, Kenya.

Nani anafanya utafiti huu?

Utafiti huu unaendeshwa na shirika la Médecins Sans Frontières, ambalo wakati mwingine hujulikana kama Madaktari Wasio na Mipaka (lililoko Corral Drive Nyali, Mombasa). Utafiti unaendeshwa kwa ushirikiano na Idara ya Afya ya Kaunti ya Mombasa. 

Watafiti wakuu ni Dkt Denton Callander na Patricia Owira. Watafiti wengine wa utafiti huu ni pamoja na Celina Kithinji na Ahmed Adam (Idara ya Afya ya Kaunti ya Mombasa), Dkt Makobu Kimani (Taasisi ya Utafiti ya Medican Kenya), na Dkt Iza Ciglenecki, Kelly Khabala, Khidir Musa, & Nitya Udayraj (Médecins Sans Frontières).  

Je, ushiriki utahusisha nini?

Kushiriki katika mradi huu ni kwa hiari kabisa. Ikiwa hutaki kushiriki, sio lazima.

Ukiamua kushiriki, utaombwa ukamilishe utafiti wa siri mtandaoni, ambao unapaswa kuchukua kati ya dakika 5-15. Utafiti utakuuliza maswali kuhusu afya na ustawi wako, uhusiano wa kingono na kimapenzi, matumizi ya dawa za kulevya na pombe, na mitazamo, imani na maarifa yako. Inaweza pia kukuuliza baadhi ya maswali yanayoweza kuwa nyeti, ikijumuisha kuhusu matukio ya unyanyasaji, uavyaji mimba. Unaweza kuchagua kuruka maswali haya ukipenda.

Hakuna taarifa yoyote utakayopeana inayoweza kuhusishwa na wewe binafsi na majibu ya washiriki yatashughulikiwa kwa usalama na usiri wa hali ya juu.

Je, kuna hatari zozote zinazohusiana na utafiti huu?

Kwa ujumla, kuna hatari chache zinazohusika na kushiriki katika utafiti huu. Inawezekana kwamba ukahisi kufadhaika utakapokumbuka mambo flani yaliyopita, hasa ikiwa mambo hayo hayakuwa mazuri. Tafadhali jua kwamba una chaguo la kusitisha ushiriki wakati wowote au kuruka maswali ambayo ungependelea kutojibu.

Iwapo wakati wowote wa utafiti unahisi hitaji la kuzungumza na mtu, unaweza kubofya kitufe cha 'Je, unahisi kufadhaika' kilicho juu ya skrini yako. Kubofya kitufe hiki kutakupa baadhi ya chaguo za kuzungumza na mshauri wa kitaalamu.

Je, nitanufaika vipi kwa kushiriki kwenye utafiti huu?

Ingawa kushiriki hakutakunufaisha moja kwa moja, ukikamilisha utafiti utapewa nafasi kushiriki kwenye mchezo wa bahati nasibu ambapo zawadi za kushindaniwa ni kama muda wa maongezi kwenye simu, tikiti za filamu na zaidi. Kwa ujumla zaidi, tunatarajia matokeo ya utafiti huu yatasaidia kuboresha afya na huduma za afya kwa Vijana na Makundi Maalum mjini Mombasa.

Je, ikiwa ninataka kujiondoa kwenye utafiti?

Kama ilivyotajwa, ushiriki katika utafiti huu ni wa hiari kabisa. Unaweza kuchagua kujiondoa wakati wowote kwa kufunga dodoso, ambapo hilo halitaathiri kwa njia yoyote uhusiano wako na Médecins Sans Frontières au washirika wengine wowote wa utafiti.

Ukijiondoa kwenye utafiti tutaharibu taarifa zozote ambazo tayari zimekusanywa. Hata hivyo, baada ya kuwasilisha dodoso, hatutaweza kuondoa majibu yako kwa kuwa dodoso halina jina.

Je, ni nini hufanyika na taarifa zinazonihusu? 

Kukamilisha utafiti ni dalili kwamba umepeana idhini ya kushiriki katika utafiti huu. Washiriki wakuu pekee wa timu ya utafiti walioidhinishwa na watafiti wakuu ndio wataweza kufikia data utakayotoa, ambayo hatutawahi kushiriki na mtu mwingine yeyote (ikiwa ni pamoja na wazazi au walimu wako!).

Tutatumia maelezo utakayotoa kufanya uchanganuzi kadhaa unaohusiana na afya na ustawi wa Vijana. Matokeo yatashirikiwa kwenye mitandao ya kijamii na kupitia machapisho ya kitaaluma, mawasilisho na ripoti. Katika zote hizo, taarifa itawasilishwa kwa namna ambayo haitawezekana kukutambua wewe au washiriki wengine wowote mmoja mmoja.

Je, tutapata kufahamu kwa njia ipi matokeo ya utafiti huu?

Matokeo ya utafiti yatashirikiwa kwa njia ambayo haitakutambulisha kwa jina lako kupitia mitandao ya kijamii. Pia yatapatikana kwenye tovuti ya utafiti: www.mombasayouthstudy.com Ikiwa unataka, mwishoni mwa utafiti unaweza kubainisha kupokea arifa wakati matokeo yako tayari.

Je, nifanye nini ikiwa ninataka kujadili utafiti huu zaidi?

Je, ungependa kujifunza zaidi? Tazama video hii, ambayo inaelezea mradi huo kwa undani zaidi. Unaweza pia kuwasiliana na timu ya utafiti moja kwa moja ili kuuliza maswali yoyote ambayo unaweza kuwa nayo. Tupigie tu kwenye WhatsApp (+254 110 064 465) au kupitia barua pepe (info@mombasayouthstudy.com).

Je, niwasiliane na nani ikiwa nina mahangaikio kuhusu utafiti huu?

Utafiti huu umeidhinishwa na Kitengo cha Ukaguzi wa Maadili ya Kisayansi cha Taasisi ya Utafiti wa Matibabu ya Kenya (Scientific Ethics Review Unit of the Kenya Medical Research Institute). Ikiwa una mahangaiko au malalamiko yoyote kuhusu utafiti huu, unapaswa kuwasiliana na Mratibu wa Maadili ya Utafiti wa Kibinadamu kupitia kwa +254 717 719 477 au seru@kemri.org na nukuu nambari ya kumbukumbu ambayo ni 4694.

Asante kwa kuchukua muda kushiriki utafiti huu.

Pakua habari hii.